CHANZO CHA MIGOGORO KATIKA FAMILIA
Ndugu wa mume au mke mara nyingi huwa ndio chanzo cha migogoro katika ndoa. Lakini kuna njia kadhaa za kudumisha uhusiano mzuri baina yako na wao. Kati ya mbinu nyingi bora, zifuatazo ni baadhi ya dondoo za kusaidia :
1). Kumbuka wazazi wa mwenza wako wa ndoa wanamjua vizuri na wamempa upendo mkubwa kwa muda mrefu kabla ya wewe kukutana naye au kuoana naye. Kamwe usianze kuzusha ugomvi kwa kumwambia chagua kati “yangu au wao”. Kumbe, ana haki ya kuonesha upendo kwa wazazi na walezi wake na hii ni sehemu ya utekelezaji wa Amri ya Mungu na wajibu wa watoto kwa wazazi wao!
2). Iwapo katika familia ya mumeo kuna migogoro na ugomvi, acha pande husika zishughulikie matatizo na migogoro yao. Kama mama mkwe ana tatizo na baba mkwe wako, waache wayamalize wao wenyewe. Wewe tumia busara ya kukaa pembeni. Usiingilie katika ugomvi wao. Kumbuka daima wagombanao ndio wapatanao, ukijiweka kimbelembele, siku moja utaumbuka wakipatana na kushibana tena!
3). Usimwamulie mwenza wako jinsi ya kuboresha uhusiano na wazazi wake. Yeye anajuana nao vizuri. Sikiliza kwa makini ili kutotia petroli katika moto uwakao. Uwe na ushauri wa busara katika mahusiano ya wenza wako wa ndoa na wazazi wake
4). Tegemea mabadiliko katika muda wako kwa ajili ya wazazi wako kwa sababu ya uhusiano mpya wa ndoa. Wewe umepokonya uhusiano wa damu na kuanzisha uhusiano wa ndoa. Wazazi watapenda uendelee kama mtoto wao na kamwe usikue hata siku moja.
5). Kumbuka kuwa mara nyingi mama huwa na wasiwasi kuhusu mke wa mwanaye na baba huwa na wasiwasi na hofu juu ya mume wa binti yake.
6). Daima vumiliana na ndugu wa mwenza wako kwa huruma, heshima na kujali. Ujue nafasi yako ni kama daraja kwao.
7). Weka mizania kati ya mahitaji yako na mahitaji ya ndugu wa mumeo/mkeo. Upande mmoja usizidi na kuelemea kwa kupitiliza.
8). Kamwe usimlinganishe mkeo na mamako au mumeo na babako.
9). Usipeleke ugomvi wenu kwa wazazi wako.
10). Kama unawapa msaada wa kifedha wazazi wako, ni vizuri kuwa wazi na mtaarifu mwenzako kama sehemu ya kuonesha uwazi na kuonesha kuwa unamheshimu.
11). Usimkataze mwenzako kuitembelea familia yake. Kabla ya kumjua na kuanza kuishi yake ufahamu wazi alitoka katika familia hiyo.
12). Usianike siri zenu kwani hata nguo chafu zinaanikwa ndani ya nyumba
13). Panga muda wa kuwafahamu ndugu wa mumeo/mkeo lakini kaa mbali na migogoro yao, usije ukabebeshwa mzigo usiokuhusu!
14). Chunga adabu na heshima unapokuwa na shemeji zako; yaani usiwakumbatie au kuwabusu. Sio lazima kila mwisho wa juma kukaa pamoja na ndugu wa mumeo/mkeo. Wape fursa babu na bibi kuwaona na kucheza na wajukuu zao kwani wao wao ni chemchemi ya hekima na busara; wanaweza pia kusaidia kurithisha imani na tunu za maisha ya kiutu na kitamaduni kwa vijana wa kizazi kipya.
15). Jitahidi kuwa mtu wa kusamehe na dumisha tabia yako ya ucheshi.
16). Kumbuka kuwa hakuna awezaye kuingia au kuathiri ndoa yako mpaka utakapompa fursa ya kufanya hivyo.
17). Kama iliwezekana waalike ndugu wa mume/mke wako angalau mara moja kwa mwezi kwa ajili ya chakula. Watembelee kila unapoweza na mshajiishe mwenzako kuwatembelea wazazi mara kwa mara na kuwajulia hali. Kwa njia hii mtaweza kujenga madaraja ya ukarimu na upendo; mtaweza kufahamiana wakati wa raha na kusaidiana kwa dhati wakati wa shida
18). Wazazi wanapofikwa na uzee na wakawa wanawategemea, basi zungumzeni kama wanandoa na mpange na kuratibu namna nzuri ya kuwasaidia. Kamwe msiwatelekeze wazazi wenu kwani watoto wanao wajibu na dhamana kubwa kwa wazazi wao. Onesha adabu na heshima kwa wazee ambao wamepungukiwa katika uzee wao au kutokana na ugonjwa! Kanuni hizi zinalenga kusaidia kujenga na kudumisha familia bora.
No comments: